Tuesday, May 2, 2017

LIGI KUU YA VODACOM BARA KUENDELEA JUMAMOSI, JUMAPILI

Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inatarajiwa kuendelea Jumamosi Mei 6 na Jumapili Mei 7, mwaka huu kwa jumla ya michezo sita.
Kwa mujjibu wa ratiba, michezo ya Jumamosi kutakuwa na michezo mitano ilihali Jumapili kutakuwa na mechi moja.
Michezo ya Jumamosi itakuwa ni kati ya Toto African na JKT Ruvu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati Majimaji ya Songea itakuwa mwenyeji wa Mwadui kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.
Kagera Sugar itaalikwa na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani wakati Young Africans ya Dar es Salaam itaialika Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Siku hiyo ya Jumamosi Mei 6, mwaka huu Azam FC itaialika Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Mbagala, Dar es Salaam ilihali Jumapili kutakuwa na mchezo kati ya Simba SC na African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wakati mechi zote zitaanza saa 10.00 jioni, mchezo kati ya Azam na Mbao utaanza saa 1.00 usiku.


 

SERENGETI BOYS YAPANGIWA LIBREVILLE
Timu ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti Boys, imebadilishiwa kituo kutoka Port Gentil na sasa imepangiwa Libreville.
Serengeti Boys imepangwa kundi B pamoja na timu za Niger, Angola na Mali ambako watafungua nayo mchezo Mei 15, mwaka huu. Kwa mabadiliko hayo, Kundi A lenye timu za Cameroon, Ghana, Guinea pamoja na wenyeji Gabon, litakuwa Port Gentil.

Kwa sasa Serengeti Boys wako Cameroon kwa kambi ya wiki moja iliyoanza Aprili 29, mwaka huu ambako tayari imecheza na wenyeji Cameroon mchezo mmoja na kushinda bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika jijini Yauonde.

Wenyeji hao, Cameroon watarudiana na Serengeti Boys katika mchezo mwingine wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika kesho Jumatano, Mei 3, mwaka huu.
……………………………………………………………

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA