Wednesday, May 31, 2017

MANCHESTER UNITED NDIO KLABU YENYE THAMANI KUBWA ULAYA – KPMG!

Manchester United ndio Klabu yenye Thamani kubwa Ulaya kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa na Magwiji wa Biashara, KPMG.
Utafiti wa KPMG umeonyesha Man United, ambao ni Mabingwa wa UEFA EUROPA LIGI, wapo mbele ya Klabu Vigogo za Spain, Real Madrid na Barcelona wakiwa na Thamani ya Euro Bilioni 3.09.
Utafiti huo ulichunguza Haki za Matangazo na Mapato yatokanyo, Faida, Umaarufu, Uwezo Kimichezo na Umiliki wa Viwanja.
Utafiti huo ulipitia Mahesabu ya Klabu 32 huko Ulaya na 6 kati ya zile 10 Bora zinatoka England.
Mahesabu yaliyopitiwa ni yale ya Misimu ya 2014/15 na 2015/16.
Mkuu wa Michezo wa KPMG, Andrea Sartori, ambae ndie Mwandishi wa Ripoti ya Utafiti huu, amesema Kibiashara Sekta ya Soka imekua mno kwa Mwaka Mmoja uliopita.
Kuhusu Haki za Matangazo, Sartori amesema England inaongoza kwa mbali mno kwenye Mapato ya eneo hili.

10 BORA kwa Thamani Ulaya:
Manchester United – Euro Bilioni 3.09
Real Madrid - 2.97
Barcelona - 2.76
Bayern Munich - 2.44
Manchester City - 1.97
Arsenal - 1.95
Chelsea - 1.59
Liverpool - 1.33
Juventus - 1.21
Tottenham - 1.01
Chanzo: KPMG

Kwa mujibu wa KPMG, Mwaka huu Klabu 10 zimewezwa kuvuka Thamani ya Euro Bilioni 1 huku Tottenham Hotspur na Juventus zikitinga 10 Bora kwa mara ya kwanza.
Tottenham imeing’oa Klabu ya France Paris Saint-Germain kutoka Nafasi ya 10 na kukaa wao.
Licha ya England kuwa na Klabu 6 kwenye 10 Bora, Spain ndio Nchi pekee yenye Klabu 2 zenye Thamani ya Zaidi ya Euro Bilioni 2.