Friday, June 2, 2017

JUVENTUS STADIUM KUBATIZWA ALLIANZ STADIUM

MABINGWA wa Italy Juventus wamesaini Mkataba wa kubadili jina la Uwanja wao ambao sasa utaitwa Allianz Stadium kuanzia Julai Mosi.
Juve wamesaini Mkataba huo wa kubadili Jina la Uwanja kutoka Juventus Stadium ulioko Jijini Turin, Italy na Jina kuwa Allianz Stadium litadumu hadi 2023.

Mkataba huo umesainiwa na Kampuni ya Bima ya Kimataifa ya Allianz pamoja na Lagardere Sports wanaomiliki Majina ya Viwanja.
Kampuni ya Allianz pia inadhamini Viwanja vingine vikubwa sehemu nyingi Duniani ikiwa pamoja na cha Mabingwa wa Germany Bayern Munich kilichopo Jijini Munich, Germany kinachoitwa Allianz Arena na kile cha Klabu ya France, Nice, kiitwacho Allianz Riviera.

Uwanja huu wa Juventus ulifunguliwa rasmi Septemba 8 Mwaka 2011 na unapakia Watazamaji 41,507.

Juve ndio Mabingwa wa Italy kwa Misimu 6 mfululizo na pia Msimu huu wametwaa Coppa Italia na Jumamosi hii wanasaka Trebo kwani watacheza Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI dhidi ya Mabingwa Watetezi Real Madrid huko Cardiff, Wales.