Wednesday, June 14, 2017

MANCHESTER UNITED YAMSAJILI VICTOR LINDELOF KWA £30.7m


MANCHESTER UNITED imekamilisha kumsaini Beki Victor Lindelof kutoka Benfica ya Ureno kwa Dau la Pauni Milioni 31.
Mchezaji huyo wa Kimataifa wa Sweden mwenye Miaka 22 alitua Jiji la Manchester Jana kupimwa Afya na kuafiki Maslahi Binafsi na Jana Dili ilikamilika baada ya mambo yote kwenda sawa na kusaini Mkataba wa Miaka Minne na Kipengele cha Kuongeza Mwaka Mmoja juu yake.
Mkataba huu unaanza rasmi Julai Mosi wakati Dirisha la Uhamisho litakapofunguliwa rasmi.
Lindelof, ambae ameichezea Sweden mara 12, sasa anakuwa ndie Beki alienunuliwa kwa Bei ghali na Man United tangu walipolipa Pauni Milioni 29.1 kumnunua Rio Ferdinand Mwaka 2002.

Victor Lindelof alijiunga na Benfica Mwaka 2012 akitokea Klabu ya kwao Sweden Vasteras SK na Msimu uliopita aliichezea Benfica mara 47 ikitwaa Dabo, Ubingwa na Kombe la Ureno.

Akiongea mara baada ya kusaini Mkataba, Lindelof alisema: “Nimefurahishwa mno. Nilifurahia muda wangu na Benfica na kujifunza mengi. Lakini sasa nangojea kwa hamu kucheza Ligi Kuu ndani ya Old Trafford na chini ya Jose Mourinho. Nipo tayari kuanza na kuchangia kwa Timu kutwaa Mataji.”
Nae Meneja Jose Mourinho ametamka: “Victor ni Kijana mwenye Kipaji kikubwa ambae mbeleni mwake ni kuzuri. Msimu uliopita ulituonyesha tunahitaji kuongeza nguvu na Vipaji kwenye Kikosi na Victor ni wa kwanza kujiunga!”

WACHAMBUZI:
Baadhi ya Wachambuzi wamedai Manchester United imekuwa ikipwaya kwenye idara ya Masentahafu tangu alipostaafu Meneja Sir Alex Ferguson Mwaka 2013.
Msimu uliopita, kuna kipindi sehemu hiyo ilitulia walipocheza pamoja Phil Jones na Marcos Rojo hadi ikamfanya Mourinho asimnunue Victor Lindelof Mwezi Januari.
Lakini wote wakaumia pamoja na Chris Smalling na ikabidi Daley Blind ajaze nafasi hiyo.

Akiwa na Urefu wa Futi 6 Inchi 2, Lindelof ni Jabali kwenye ngome na Umri wake wa Miaka 22 unamfanya awe Kijana zaidi kupita Rio Ferdinand alipojiunga na Man United Mwaka 2002 kutoka Leeds United.

Wachambuzi hao wanadai ikiwa Lindelof ataiga kiasi tu ya yale Rio aliyomletea Ferguson basi Mourinho atakuwa amepata Pacha safi mno wa Eric Bailly.