Wednesday, July 26, 2017

ALVARO MORATA AANZA MECHI YAKE YA KWANZA CHELSEA, CONTE ASEMA ANAHITAJI MUDA!


JANA Alvaro Morata alianza kuichezea Chelsea kwa mara ya kwanza walipofungwa 3-2 na Bayern Munich huko Singapore.
Kwenye Mechi hiyo, Mchezaji huyo wa Kimataifa wa Spain aliingizwa katika Dakika ya 63 na mchango wake mkubwa ni kusaidia kupatikana Bao la Pili la Chelsea katika Dakika ya 85 mfungaji akiwa Michy Batshuayi.
Meneja wa Chelsea Antonio Conte amekiri Alvaro Morata anahitaji muda zaidi ili kujiiingiza kwenye staili ya uchezaji wa Mabingwa hao wa England.
Jana, alipoingizwa Morata alicheza kwenye Fowadi ya Mtu 3 yeye akiwa pembeni Kushoto, Batshuayi akiwa Kati na Willian pembeni Kulia huku Chelsea wakitumia Mfumo aupendao Conte wa 3-4-3.
Mbali ya kuchangia Bao la Batshuayi, Morata hakujaribu Shuti lolote Golini ingawa alionyesha umahiri wake mkubwa wa kuburuza Mpira kutoka katikati ya Uwanja kuongoza mashambulizi ya Timu yake.
Akiwa na Real Madrid, Morata, mwenye Umri wa Miaka 24, alikuwa akichezeshwa Fowadi Kati lakini mara nyingi alitupwa Kushoto.

Jana Conte alimtupa Kushoto na pia kumtaka awe anatumbukia Kati kila unapotokea mwanya ili kumsaidia Batshuayi.
Kwa sasa Chelsea haina Staa wao Eden Hazard anaeuguza Majeruhi yake na pengine hatarajea hadi Septemba.
Katika kipindi cha kukosekana kwa Hazard, inadhaniwa Conte atatumia Fowadi hiyo hiyo ya Mtu 3 ya Morata kuwa pembeni Kushoto, Batshuayi akiwa Kati na Willian pembeni Kulia
Bila shaka Hazard akirejea, Morata atarudishwa Kati na Hazard kucheza pozisheni yake ya kawaida ya upande wa Fowadi Kushoto.
 

NINI CONTE KASEMA:
Conte, alivutiwa na uchezaji wa Morata, na ameeleza: "Lazima tumpe muda zaidi kujisuka kwenye staili yetu ya Uchezaji. Ni wazi atafurahia uchezaji wake katika Mechi yake ya kwanza!"
Aliongeza: "Ni ngumu kueleza mchango wa Morata kwa sasa kwani tumekuwa nae kwa Siku 2 tu. Inabidi afanye kazi zaidi na kuelewa mfumo wetu. Lakini ameonyesha nia thabiti na yeye ni Mchezaji mzuri mno tuliemnunua!"