Wednesday, July 12, 2017

BORUSSIA DORTMUND YAWATEGA CHELSEA KWA AUBAMEYANG, YAWATAKISHA PAUNI MILIONI 70!

Chelsea wamepewa Ofa ya kumsaini Straika wa Borussia Dortmund Pierre-Emerick Aubameyang kwa Dau la Pauni Milioni 70 kwa mujibu ya vyanzo vya Sky Sports TV ya huko Uingereza.
Chelsea hivi sasa wanahaha kumsaka Sentafowadi baada ya Meneja wao kumtosa Diego Costa na wao kumkosa mlengwa wao Romelu Lukaku.
Hilo limewafanya wawalenge Mafowadi wengine akiwemo Alvaro Morata wa Real Madrid.
Mbali ya Chelsea kupewa Ofa hii na BVB, Sky Sports imetoboa kuwa hata AC Milan ya Italy wapo Mazungumzoni na BVB kuhusu kumnunua Staa huyo wa Gabon huku pia Paris Saint-Germain ikitaka nayo kujitumbukiza kumwania.
Aubameyang alianza Soka lake na Milan lakini hakuwahi kuchezea Timu ya Kwanza na kutolewa nje kwa Mkopo.
Msimu uliopita, Aubameyang alipachikia Bao 42 kwa BVB na Nchi yake Gabon. 

Tangu ajiunge na BVB kutoka Saint-Etienne ya France Mwaka 2013 Aubameyang mwenye Miaka 28 amefunga Bao 85 kwenye Bundesliga katika Mechi 128 alizocheza.
Mchezaji huyo amebakiza Miaka Mitatu katika Mkataba wake na Dortmund.