Saturday, July 15, 2017

CHAN 2017/18: LEO CCM KIRUMBA, MWANZA, TANZANIA vs RWANDA

LEO Timu ya Taifa ya Tanzania, maarufu kama Taifa Stars, itajimwaga Jijini Mwanza ndani ya CCM Kirumba Stadium kuivaa Rwanda, maarufu kama Amavubi, katika Mechi ya Raundi ya Pili ya Mashindano ya CAF ya Mataifa ya Afrika, CHAN, ambayo hushirikisha Wachezaji wanaocheza Ligi za ndani za Nchi zao tu.
Jumla ya Nchi 48 zinashiriki CHAN na zimegawanywa katika Kanda ambapo Washindi 15 watajumuika na Wenyeji Kenya kucheza Fainali hapo Mwakani.
Tanzania ipo Kanda ya Afrika ya Kati na Mashariki ambayo ina Nchi 9 na itatoa Timu 2 kucheza Fainali.
Kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga, ameahidi Kikosi chake kupambana kweli kweli ili kuleta ushindi wa Nyumbani.
Mayanga amesisitiza kuwa Kikosi chake, ambacho Wiki iliyopita kilishika Nafasi ya 3 katika Mashindano ya COSAFA huko Afrika Kusini, kina ari na morali kubwa.

Nao Rwanda, chini ya Kocha Antoine Hey, ambae aliwahi kuzifundisha Nchi za Gambia na Lesotho, amehuzunika na matayarisho ya Timu yake ambayo hata kutua kwao Jijini Mwanza hapo Jana kulikuwa kwa taabu kwani walitua hapo kwa mafungu kutokana na kadhia ya usafiri.
Rwanda walitakiwa kufika Mwanza tangu Juzi.
Mbali ya kukerwa na hilo, Kocha Hey amesema wapo imara licha ya kuwa na Kikosi kichanga ingawa alalamikia hali mbaya ya Uwanja wa kuchezea wa CCM Kirumba.

Viingilio vya Mechi hii hko CCM Kirumba ni Shilingi 5,000 na 10,000.