Monday, July 24, 2017

CHICHARITO KUPIMWA AFYA ILI ATUE WEST HAM

Javier Hernandez, maarufu kama Chicharito, ataruka kwenda London Jumanne kupimwa Afya yake na kukamilisha Dili ya kuhamia West Ham.
Chicharito, mwenye Umri wa Miaka 29 na ambae huchezea Timu ya Taifa ya Mexico, atakuwa ndie Mchezaji Kihistoria atakaelipwa Mshahara mkubwa huko West Ham akizoa kitita cha £140,000 kwa Wiki.
Wiki iliyopita West Ham iliafikiana na Klabu ya Chicharito Bayer Leverkusen na kisha kutoa taarifa rasmi kuthibitisha Uhamisho huo.

Kabla kuuzwa huko Germany kwa Bayer Leverkusen, Chicharito alikuwa na Manchester United kati ya 2010 na 2015 akifunga Bao 59 katika Mechi 156 na kutwaa Ubingwa wa England mara 2 na Msimu wa 2014/15 kupelekwa Real Madrid kwa Mkopo.
Agosti 2015 Chicharito aliuzwa kwa Leverkusen ambako alipiga Bao 39 katika Mechi 76.
Fowadi huyu ameichezea Mexico Mechi 96.
Hadi sasa, katika Dirisha la Uhamisho la sasa, West Ham wamesaini Wachezaji Watatu ambao ni Mchezaji wa Stoke City Marko Arnautovic, aliesainiwa kwa Dau la Rekodi ya Klabu, Pablo Zabaleta, kama Mchezaji Huru kutoka Man City na Kipa wa Man City Joe Hart aliejiunga kwa Mkopo wa Msimu Mmoja.