Friday, July 14, 2017

MANCHESTER UNITED NA CITY KUVAA NEMBO YA NYUKI KUWAENZI WAHANGA WA MLIPUKO!

TIMU za Manchester United na City zitawaenzi Wahanga wa Mlipuko wa Bomu uliotokea Manchester Arena kwa kuvaa Jezi zenye Nembo ya Nyuki katika Mechi kati yao.
Baada ya Mechi hiyo Jezi hizo zitapigwa Mnada ili Mapato yake yaende kwenye Mfuko wa Hisani wa Kusaidia Wahanga wa Maafa hayo uitwao We Love Manchester Emergency Fund.
Mfuko huo umeshakusanya Zaidi ya Pauni Milioni 12 kusaidia Maafa hayo yaliyotokea Mei 22 na kuua Watu 22.
Man United na City zitavaa Jezi zenye Nembo ya Nyuki kwenye Dabi yao itakayochezwa Julai 20 huko Houston, USA ikiwa ni Dabi ya kwanza kati yao kuchezwa nje ya England.
Nembo ya Nyuki imekuwa ndio Alama ya Mshikamano kwa Watu wa Jiji la Manchester na imetumika sana tangu Maafa hayo huku wengine wakijichora Miilini mwao kwa Tattoo.

Imeeleza ‘Nyuki Mfanyakazi’ ndio Alama ya Asilia ya Jiji la Manchester tangu zama za Karne zilizopita ikisisitiza Jiji la Wafanyakazi wa kawaida waliohenya kulijenga Jiji hilo.
Mtendaji Kuu wa Man City, Soriano, ameeleza: “Alama ya Nyuki Mfanyakazi ni alama inayoonyesha kila kitu kuhusu Manchester na Wachezaji wetu watavaa Nembo ya Nyuki kwa fahari kubwa na mshikamano kwa Jamii ya Manchester.”

Nae Ed Woodward, Mwenyekiti Mtendaji wa Man United, ameeleza Jiji la Manchester limeonyesha nguvu na umoja tangu mashambulizi hayo ya Mabomu na kuionyesha Dunia kwamba Mji huo ni spesho.
Aliongeza: “Kwa kuvaa Nembo ya Nyuki, tutaonyesha ari ya Jamii yetu katika Mji wetu na Klabu zetu!”