Thursday, July 13, 2017

UHAMISHO 2017: CHELSEA, MONACO ZAAFIKI DILI YA KUUZIANA BAKAYOKO £40M, SASA MATIC KWENDA MAN UNITED

Chelsea wamekubali kuilipa AS Monaco Pauni Milioni 40 ili kumnunua Kiungo Tiemoue Bakayoko.
Bakayoko, mwenye Miaka 22, atapimwa Afya huko Stamford Bridge kabla Wikiendi hii kuanza ili kukamilisha taratibu za Uhamisho.
Dili hii ilikuwa Mezani kitambo lakini imesuasua mno hasa kutokana na Mchezaji huyo kutopona haraka Goti lake alilopasuliwa mwishoni mwa Msimu uliopita.
Bakayoko aliichezea AS Monaco Mechi 51 Msimu uliopita na kuisaidia kutwaa Ubingwa wa France kwa mara ya kwanza baada ya Miaka 17.

Mbali ya Ubingwa huo, AS Monaco pia ilifika Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI huku Bakayoko akiwa nguzo imara kwao.
Kutua kwa Bakayoko huko Stamford Bridge kunaweza kufungua njia kwa Kiungo wa Chelsea Nemanja Matic kuondoka Klabuni hapo.
Inaaminika mwenyewe Matic anataka kwenda Man United kuungana tena na Jose Mourinho aliemleta Mchezaji huyo hapo Chelsea wakati akiwa Meneja.

Lakini inasemekana Chelsea haipendi kumuuza Matic kwa Man United hasa baada ya kupokwa kwa mlengwa wao Romelu Lukaku kutoka Everton na Fowadi huyo kutua Old Trafford badala ya Stamford Bridge.