Saturday, August 12, 2017

ODEN MBAGA BOSI MPYA WA WAAMUZI TANZANIA

Oden Mbaga (katikati) akiwa na Hamis Changwalu (kulia) na Omar Kambagwa enzi akichezesha soka
MWAMUZI wa mstaafu wa soka wa Kimataifa Oden Mbaga amechaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Waamuzi Taifa (FRAT) katika Uchaguzi uliofanyika juzi Dodoma.
Katika uchaguzi huo nafasi ya Katibu ambayo iligombewa na watu watatu ililazimika kurudiwa baada ya awali Mbaga kupata kura ambazo hazikufika nusu ya wajumbe.
Mbaga alipata kura 18 Abdallah Mitole kura 16 huku Jovin Ndimbo akiambulia kura mbili.
Ili kupatikana mshindi ikalazimika kupigwa kura kwa wagombea wawili ambapo Mbaga alipata kura 21 na Mitole akipata kura 15
Mwenyekiti alichaguliwa Joseph Mapunda kwa kura 36 na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF alichaguliwa Alanus Luena kwa kura 21.
Akizungumza na gazeti hili, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi huo, Benjamini Kalume alisema jumla ya wajumbe 36 walihudhuria na kupiga kura.
“Uchaguzi ulifanyika vizuri na niwashukuru wajumbe kwa kuonesha ukomavu kwani hakuna kura iliyoharibika lakini pia uongozi uliochaguliwa uitishe uchaguzi mapema ili kuziba nafasi ambazo hazikupata wagombea,” alisema Kalume.
Naye Katibu mpya wa FRAT, Mbaga aliwashukuru wajumbe kwa kujenga uaminifu kwake na kuahidi kuona FRAT mpya ambayo itajenga waamuzi na kuwatetea.