Sunday, August 27, 2017

SIMBA SC YATOA ONYO, OKWI APIGA HAT TRICK IKIIBUKA NA MABAO 7-0.

SIMBA imetoa onyo katika Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting kwa mabao 7-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam
Mchezo huo ni moja ya mechi saba za ligi hiyo zilizochezwa ikiwa ni ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mwaka 2017/18, huku mabingwa hao wa Kombe la FA na Ngao ya Jamii wakitoa kichapo cha nguvu.
Mchezaji mpya wa Simba, Emmanuel Okwi ndiye alikuwa shujaa katika mchezo huo baada ya kutupia mabao manne na kuondoka na mpira katika mchezo huo huku akiwa mchezaji wa kwanza kufunga `hat-trick’ msimu huu.
Okwi alifunga bao la kwanza katika dakika ya 18 akipokea pasi ya Mzamiru Yasini kabla ya kufunga la pili katika dakika ya 22 huku la tatu lililomhakikishia kuondoka na mpira akilipachika katika dakika ya 35.
Kichuya aliifungia Simba bao la nne na tano lilifungwa na Juma Luizio huku Simba ikimaliza kipindi cha kwanza ikiwa mbele kwa mabao 5-0 dhidi ya Ruvu Shooting baada.


Katika kipindi cha kwanza Ruvu walimtoa Chande Magoja na kuingia Zuber Dabi katika dakika ya 38, Haruna Niyonzima alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Mohamed Ibrahim kwa upande wa Simba katika dakika ya 41.
Dakika ya 52, Okwi aliifungia Simba bao la sita akipokea pasi kutoka kwa Said Ndemla aliyeingia kipindi cha pili. Ndemla aliingia kuchukua nafasi ya Mzamiru Yasini.
Nyoni aliifungia Simba bao la saba katika dakika ya 81 na kuihakikishia timu hiyo ushindi wa mabao 7-0 ikiwa ya kwanza kukalia uongozi wa ligi hiyo baada ya kuwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga.
Naye Alexander Sanga anaripoti kutoka Shinyanga kuwa; wenyeji Mwadui waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi Singida United kwenye Uwanja wa Mwadui Complex.
Mabao ya Mwadui yalifungwa na Paulo Nonga katika dakika ya 30 na Salim Khamis kwa kichwa katika dakika ya 58 akiunganisha krosi ya Hassan Kabunda. Singida ilipata bao la kufutia machozi katika dakika ya Ken Ally katika dakika ya 52.
Nayo Mtibwa Sugar iliifunga Stand United kwa bao 1-0 katika mchezo mwingine kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani huku Azam FC ikishinda 1-0 mjini Mtwara dhidi ya Ndanda FC.
Katika mechi zingine; Kagera Sugar imefungwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mbao, timu ngeni ya Njombe Mji ikichapwa 1-0 na Prisons na Mbeya City ikiifunga 1-0 Maji Maji ya Songea.