Sunday, August 20, 2017

WANACHAMA SIMBA WARIDHIA MABADILIKO

WANACHAMA 1,216 wa Simba wamepitisha uamuzi wa klabu yao kuingia kwenye mfumo wa hisa kwa kura za wazi huku mmoja pekee akipinga.
Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere ulikuwa na ajenda tisa lakini ajenda kuu zilikuwa tatu ambazo zilihusu mabadiliko ambayo ni kuwasilisha mapendekezo kwa wanachama, kujadili na kupiga kura kama mfumo huo utakubaliwa ama kukataliwa.
Katika mkutano huo ambao umehudhuriwa na wanachama 1217, wanachama 1216 walikubali wawekezaji kumiliki asilimia 50 na wenyewe kubaki kuwa wamiliki kwa asilimia 50 huku mmoja pekee akikataa baada ya kuhojiwa na Kaimu Rais wa Simba Salim Abdallah ‘Try Again’,
Pia Salum Abdallah alisema wawekezaji mmoja, wawili au watatu watatakiwa kutoa Sh bilioni 20 katika uwekezaji huo sawa na wanachama.
“Kwa sababu wanachama wanaonekana si wenye uwezo wa kutosha kifedha watatakiwa kuchangia Sh bilioni nne tu ambazo nia silimia 10 huku 40 ambayo ni sh. bilioni 16 zitawekwa kando kwa kuangalia uwezo wao,” alisema Salim Abdallah.
Kabla ya kuanza kujadiliwa agenda ya mabadiliko mwanasheria wa Simba, Evodius Mtawala aliwaeleza wanachama hao umuhimu wa kuingia kwenye mfumo huo kulingana na ibara ya 49 kifungu kidogo cha 3.

“Mtakachokiamua leo itaundwa kamati kuu huru ya wataalamu ambayo itaandaa mkutano na kuwaita kuwaeleza ni nani waliojitokeza na wanachama mtaamua ni nani atakuwa mwekezaji,” alisema Mtawala.
Pia Mtawala alisema kabla ya kuingia kwenye mchakato huo kamati ya utendaji itakaa na kuhakiki uanachama ili kupata orodha halisi ya wanachama na kuingiza kwenye leja
Naye mdhamini mpya wa Simba, Adam Mgoyi ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Kilosa aliwashukuru wajumbe kwa kumchagua kuwa mmoja wa baraza la wadhamini huku akiwa na umri mdogo.
“Nawashukuru kwa kuniamini kuwa dhamana ya kusimamia mali za klabu za Simba na nawaahidi kutokuwa na hila wala mbinafsi kwani mmenichagua baada ya kugongwa na nyoka kwani maana ya kuwa mdhamini ni kusimamia kulingana na sheria mali za klabu na nitashirikiana na wenzangu katika maamuzi mtakayofikia,” alisema Mgoyi.
“Niwashukuru viongozi kwa kuwezesha kuingia kwenye mfumo mpya kwani klabu ya Simba ina zaidi ya miaka 80 na wamefanikiwa kupitisha mabadiliko kwa kufuata utaratibu na wale ambao watakuwa hawajaelewa wanaruhusiwa kuuliza,” alimaliza Mgoyi.
Naye Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangala na Makamu wa Rais wa TFF, Wambura waliwashukuru viongozi kwa kufanikiwa kuingia kwenye mfumo na kuomba wanachama kuwa watulivu na kuahidi kutoa ushirikiano kwaq uongozi.
Mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji yalikuja baada ya mfanyabiashara, Mohamed Dewji ‘Mo’ kuonyesha nia ya kutaka kuwekeza Sh 20 bilioni huku yeye akihitaji kumiliki hisa asilimia 51 ingawa mkutano wa wanachama mmiliki wa hisa nyingi atakuwa na asilimia 50.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangala, Kaimu Rais wa Simba Salim Abdallah ‘Try Agano’, Makamu wake Idd Kajuna.

 Wengine ni wadhamini wa klabu hiyo Ramesh Patel, Adam Mgoyi na Juma Kapuya pamoja na Makamu wa Rais wa shirikisho la soka nchini (TFF), Michael Wambura ambaye ni mwanachama wa Simba.