Sunday, October 29, 2017

SIMBA NA YANGA HAKUNA MBABE, ZATOKA 1-1

TAMBO zote za watani wa jadi Yanga na Simba zimeisha kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam leo.
Timu hizo ziliingia uwanjani zikitoka kushinda mabao 4-0 katika mechi zao za mwisho, Yanga dhidi ya Stand United Shinyanga na Simba dhidi ya Njombe Mji, Uhuru, matokeo ambayo yalitoa hamu kushuhudia mechi yao ya jana kila mmoja akitaka kufahamu nani ni zaidi ya mwingine.
Wakongwe hao walianza mechi yao taratibu wakishambuliana kwa zamu na kumaliza kipindi cha kwanza suluhu.
Simba ilipata bao la kuongoza katika dakika ya 57 ambapo mchezaji wake Shiza Kichuya alifunga akiunganisha pasi ya John Bocco aliyeingia dakika ya 56 kuchukua nafasi ya Laudit Mavugo.
Bao hilo lilidumu kwa dakika tatu tu kabla Obrey Chirwa hajaisawazishia Yanga akiunganisha pasi ya Geofrey Mwashiuya.
Mechi ya jana haikuwa na shangwe nyingi kama ilivyo kawaida ya mechi za watani pengine ni kutokana na uchache wa watu waliofika uwanjani hapo kushudia mechi hiyo, tofauti na ilivyozoeleka mechi hiyo hujaza mashabiki wengi.
Aidha, muda mwingi wa mchezo wachezaji wa timu zote walionekana kucheza kwa kujilinda zaidi.
Dakika ya 22 Emmanuel Okwi alipata nafasi nzuri ya kufunga lakini mpira wake wa kichwa ulitoka nje ya goli.
Dakika moja baadaye nusura Mwashiuya aipatie Yanga bao lakini mpira wake wa kichwa ulipaa nje.
Simba ilipata tena nafasi katika dakika ya 27 ambapo mshambuliaji wake Mrundi Laudit Mavugo alishindwa kufunga baada ya shuti lake kutoka pembeni ya goli.
Dakika ya 32 Chirwa alikokota mpira mpaka kwenye boksi lakini akashindwa kufunga na mpira kupita pembeni ya goli.
Sare hiyo inairudisha Simba kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa uwiano mzuri wa mabao, huku Yanga ikishika nafasi ya pili na Azam ya tatu. Zote zina pointi 16.
Yanga: Youthe Rostand, Juma Abdul, Gadiel Michael, Andrew Vicent, Kelvin Yondani, Papy Tshitshimbi, Pius Buswita, Raphael Daud/ Pato Ngonyani, Obrey Chirwa,Ibrahim Ajibu, Geofrey Mwashiuya/ Emmanuel Martin
Simba: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jnr’, Juuko Murshid, Method Mwanjale, James Kotei/ Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Muzamiru Yassin/ Said Ndemla, Laudit Mavugo/ John Bocco, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima.