Saturday, October 28, 2017

SIMBA NA YANGA KUONESHANA KAZI KATIKA UWANJA WA UHURU PUNDE LEO


MACHO na masikio ya mashabiki wa soka leo yataelekezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam pale watani wa jadi, Yanga na Simba watakapomenyana katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mashabiki wa timu hizo wamekuwa wakitambiana kuanzia mitaani, nyumbani, katika vyombo vya usafiri, sokoni, vijiweni na kila mahali, ambapo kila mmoja akitamba kuibuka na ushindi leo.


UPINZANI MKALI
Upinzani mkali kwa timu hizo unaonekana kuongezeka baada ya Yanga kumchukua mshambuliaji hatari wa watani wao wa jadi Simba, Ibrahim Ajibu, huku Simba nao wakimchukua Haruna Niyonzima.

Wawili hao hasa Ajibu ameonesha makali na kuisaidia Yanga kupata mabao kibao, huku mchezaji huyo naye akiwania kiatu cha dhahabu kama alivyo Emmanuel Okwi wa Simba.
Ushindani mkali utakuwa kwa Ajibu na Okwi katika mbio za kupachika mabao, kwani wachezaji hao wameonesha makali yao karibu katika kila mchezo wa timu zao walizocheza.
Katika msimamo wa ufungaji, Okwi anaongoza akiwa na mabao nane na amekuwa tegemeo kubwa kwa timu yake ya Simba, hasa katika mechi zinazowakutanisha na Yanga, kwani ana rekodi nzuri ya kuwafunga wapinzani hao.


Pia Okwi amefunga katika michezo yote ya Ligi Kuu aliyocheza msimu huu hususani kwenye Uwanja wa Uhuru, ambao ndio utakaotumika kuchezewa mchezo huo wa leo.
Ajib katika msimamo wa ligi tayari ameshafunga mabao matano na ndiye mchezaji anayeongoza kwa mabao kwa Yanga na hakuna ubishi kuwa mchezaji huyo yuko katika kiwango cha juu cha uchezaji katika kipindi hiki huku akiwafunika Tambwe na Ngoma
Hivyo, kulingana na ubora wa wachezaji hao wawili ni sababu mojawapo kubwa baina timu hizi na wanatarajiwa kuwa nguzo katika mchezo huo wa aina yake na pengine kuwa na upinzani wa juu zaidi.


Mchezo wa watani wa jadi mara kadhaa wachezaji wanalaumiwa pindi timu moja inapopoteza mchezo, makocha kufukuzwa pia viongozi hushambuliwa kwa maneno makali na mtaani mashabiki wanataniana na ukiwa una hasira za karibu unaweza kujikuta unarusha ngumi kwa sababu ya hizi timu mbili.
Katika michezo saba iliyopita ya Ligi Kuu Tanzania Bara zilizokutana tangu mwaka 2014 hadi 2017, Simba imeshinda michezo miwili na Yanga imeshinda miwili na kutoka sare mitatu.


Matokeo ya mechi Yanga na Simba

28/10/2017 Yanga ?? Simba
25/02/2017 Simba 2-1 Yanga
01/10/2016 Yanga 1-1 Simba
20/02/2016 Yanga 2-0 Simba
26/09/2015 Simba 0-2 Yanga
08/03/2015 Simba 1-0 Yanga
18/10/2014 Yanga 0-0 Simba
19/04/2014 Yanga 1-1 SimbaREKODI ZA MAKOCHA

Kwa upande wa makocha, George Lwandamina hajawahi kuifunga Simba, hivyo rekodi inambeba Omog wa Simba ambaye ameiongoza timu hiyo kuifunga Yanga katika mechi nne.Mechi ya kwanza Omog ilikuwa Oktoba mwaka jana katika mchezo wa Ligi Kuu, ambapo aliiongoza Simba kupata sare ya bao 1-1 licha ya timu yake kuwa pungufu uwanjani baada ya kiungo Jonas Mkude kupewa kadi nyekundu na baadaye bao la kona ya winga Shiza Kichuya kumuokoa dakika za majeruhi.


Mchezo uliofuata wa Ligi Kuu ulikuwa Februari, ambapo aliibuka na ushindi wa mabao 2-1 licha ya timu yake kubaki tena pungufu uwanjani baada ya beki Besala Bokungu kutolewa kwa kadi nyekundu.

Mechi nyingine mbili alizocheza bila kufungwa na Yanga ni ule wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi aliposhinda kwa penalti 4-3 pamoja na mchezo wa Ngao ya Jamii wa Agosti mwaka huu akishinda kwa penalti baada ya suluhu katika dakika 90.

Swali linabaki Omog atafanikiwa kulinda rekodi yake mbele ya Yanga kwa kuibana na kushinda au kutoa sare au atashindwa kulinda na kupokea kipigo kwa mara ya kwanza tangu aanze kuinoa timu hiyo?
Katika kujiandaa na mchezo huu timu zote ziliweka kambi nje ya Dar es Salaam wakati Yanga wakiwa Morogoro, Simba ilipanda ndege hadi visiwa vya Zanzibar na wote walitarajia kurejea jana tayari kwa mchezo huo.

Tusubiri baada ya dakika 90 nini kitatokea katika mchezo huo maarufu kama Kariakoo `Derby’ ambayo ni miongoni mwa mechi kubwa tatu barani Afrika baada ya ‘Cairo Derby’ ambayo huzihusisha timu pinzani nchini Misri, Al Ahly dhidi ya Zamalek na ‘Soweto Derby’ inayohusisha timu za Orlando Pirates dhidi ya Kaizer Chiefs zote za Afrika Kusini.
 

MAKOCHA KUTIMULIWA
Mechi za Yanga na Simba zimekuwa balaa kwa makocha, kwani wakati mwingine wanajikuta wakitimuliwa kutokana na matokeo ya uwanjani kutokuwa mazuri kwa timu zao.

Hata hivyo, katika mchezo wa leo, Omog ndiye anayeonekana kuwa katika hatari zaidi ya kutupiwa virago endapo atafungwa, kwani tayari uongozi wa timu hiyo ulishawahi kumchimba mkwara kwa matokeo mabaya ya nyuma.

Tayari Simba wameshamleta nchini aliyekuwa kocha Mkuu wa Rayon Sports, Djuma Masoud kumsaidia Omog na ndiye alikuwa kocha bora wa Ligi ya Rwanda msimu uliopita, huenda akachukua Mcameroun endapo atatupiwa virago.

Kocha Omog pamoja na kukibadilisha kikosi chake na kucheza kandanda safi bado uongozi unaonesha wakati fulani kutoridhika na matokeo hayo.
Kwa upande wa Mzambia George Lwandamina wa Yanga, yeye anaonekana hayuko hatari sana kwani Yanga wameonesha kumkubali na hivyo wako tayari kumvumilia aendelee kuwepo katika kikosi chao.

Hata hivyo, uongozi na mashabiki wa timu hizo mbili huwa hawana msamaha pale wanapoona timu yao imefanywa 'kitu mbaya' na wapinzani wao wa jadi na kuwakosesha usingizi.

Viingilio katika mchezo huo vitakuwa Sh 10,000 kwa mzunguko wakati 20,000 ni kwa jukwaa kuu.