Sunday, November 19, 2017

KOCHA MKUU WA KILI STARS YA CHALENJI ALIYETANGAZWA LEO

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limemtangaza Ammy Ninje kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ ambayo inajiandaa na mashindano ya Chalenji ambayo yanatarajiwa kuanza Desemba 3-17 Nairobi.
Akizungumza leo wakati akimtambulisha, Ofisa habari wa TFF, Alfred Lucas alisema kocha huyo kesho anatarajiwa kutangaza kikosi kitakachoshiriki michuano ya kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
“Ninje siyo mgeni kwenu mmemuona kwenye benchi la Taifa Stars takribani michezo miwili, hivyo ndio atakayekiongoza kikosi cha Kilimanjaro Stars kwenye mashindano ya Chalenji yatakayofanyika Nairobi,” alisema Lucas.
Akizungumza baada ya kutambulishwa, Ninje alisema kazi ya kocha siyo kuongea bali ni kuonesha kwa vitendo kile kilichomo ndani yake, nakuomba ushirikiano kwa wadau ili timu atakayotangaza leo ifanye vizuri na hatimaye itwae kombe la Chalenji.
“Nashukuru kwa TFF kuniamini na kunikabidhi timu ya Kilimanjaro Stars ambayo imepangwa kundi A pamoja na timu za Libya, Rwanda na wenyeji Kenya,” alisema Ninje ambaye ni kocha mwenye leseni A ya UEFA.
Kabla ya kuwa kocha Ninje aliwahi kucheza soka la kulipwa katika nchi za Afrika Kusini 1996 timu za Hellenic FC na baadae Wynberg St Jones kabla ya kujiunga na Sparta Rotterdam (Mutual) FC ya China pia alicheza katika nchi za Denmark, USA, Scotland na England.
Kwa sasa Ninje mwenye taaluma ya Uhasibu anafundisha timu ya Vijana ya klabu za Hull City na Notts County na baadhi ya wachezaji maarufu waliwahi kupitia katika mikono yake ni Josh Tymon, Josh Clackstone, Harvey Rodgers, Dan James, Max Clarke, Colby Bishop, Lartey Sarpong, Luther Wilder, Jack McMillian, Montel Gibson, Alex Penny, Jordan Richards, Harry Caldwell na Rory Watson.