Sunday, December 3, 2017

JONESIA KUCHEZESHA KOMBE LA DUNIA LA WANAWAKE NA FRANK KOMBA CHAN

WAAMUZI wa Kimataifa wa Tanzania Jonesia Rukyaa ameteuliwa kuchezesha Kombe la Dunia kwa wanawake na Frank Komba ameteuliwa kuchezesha fainali za Mataifa ya Afrika (CHAN)
Akizungumza, Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Kidao Wilfred alisema Jonesia ameteuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kuchezesha fainali zijazo za Kombe la Dunia kwa wanawake (Algarve Cup) zitakazofanyika nchini Ureno, Februari, mwakani.
Pia Kidao alisema Komba ambaye ni mwamuzi msaidizi ameteuliwa kuchezesha fainali za Mataifa ya Afrika (CHAN) inayotarajiwa kuanza Januari 13 hadi Februari 4 mwakani nchini Morocco.
“Kwa sasa Komba yupo kwenye semina Misri pamoja na waamuzi wengine 44 walioteuliwa tangu Novemba 27 na leo wanatarajia kumaliza mafunzo hivyo tumuombee hili afaulu kuchezesha fainali hizo na Jonesia anatarajiwa kushiriki semina ya FIFA itakayofanyika Doha, Qatar kuanzia Februari 12- 16, mwakani,” alisema Kidao.
Jonesia ameteuliwa kupuliza filimbi katika fainali hizo ambazo hukutanisha timu mahiri zilizofanya vema katika michuano ya kila Bara ataungana na waamuzi wengine wanne kutoka Afrika ambao ni Lidya Abebe (Ethiopia), Glady Lengwe (Zambia) na Salima Mukansanga (Rwanda).
Hii ni mara ya kwanza Tanzania kutoa mwamuzi kuchezesha fainali za Dunia kwa wanawake baada ya Marehemu Hafidh Ally kuchezesha fainali za Dunia za Vijana U-16 zilizofanyika nchini Scotland mwaka 1989. 


Kwa upande wa Komba ambaye ni mwamuzi msaidizi ni mara ya pili kuchezesha fainali za Afrika, baada ya Mei mwaka huu kwenda Gabon kwenye fainali za U-17 za Afrika.
Naye Meneja wa Marefa wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), Eddy Maillet alisema waamuzi watakaochezesha fainali za Total CHAN Morocco 2018 watatajwa siku tano baada ya kozi hiyo.


“Waamuzi hawa kutoka nchi 35 wanachama wa CAF, wanawania nafasi ya kuchezesha fainali za tano za CHAN zinazokutanisha wachezaji wanaocheza kwenye ligi za nchini mwao na mafunzo yao ni yalikuwa ya nadharia na vitendo,” alisema Maillet.
Pia Maillet alisema mafunzo mapya yalikuwa ni kwenye matumizi ya Teknolojia ya picha za Video (VAR) katika kutoa maamuzi, mfumo ambao utafanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya CHAN.
Kundi A linaundwa na wenyeji, Morocco, Guinea, Sudan na Mauritania, Kundi B kuna Ivory Coast, Zambia, Uganda na Namibia, Kundi C linaundwa na Libya, Nigeria, Rwanda na Equatorial Guinea na Kundi D lina timu za Angola, Cameroon, Kongo na Burkina Faso.
Mechi ya ufunguzi na fainali zitafanyika kwenye Uwanja wa Mohamed V Complex mjini Casablanca, ambao pia ulitumika kwenye mchezo wa marudiano wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika