Monday, January 29, 2018

EMMANUEL OKWI NA BOCCO WAIPA SIMBA USHINDI, KWASI NAYE NI HABARI NYINGINE

VINARA wa Soka Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC, leo imezidi kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Simba sasa imefikisha pointi 35 baada ya kucheza mechi 15 na kumaliza mzunguko wa kwanza wakiwa pointi tano zaidi ya Azam FC iliyopo nafasi ya pili. Yanga ambayo juzi iliifunga Azam, ni ya tatu ikiwa na pointi 28.

Simba ilipata bao la kuongoza lililofungwa na John Bocco katika dakika ya 17 baada ya kuunganisha wavuni kona na Shiza Kichuya.
Bocco alifunga la pili katika dakika ya 26 akimalizia kwa kichwa krosi ya Said Ndemla.

Majimaji walinyimwa penalti ya wazi katika dakika ya 19 baada ya Juuko Murshid kumchezea rafu, Geofrey Mlawala lakini mwamuzi akasema ipigwe adhabu ndogo.

Timu hiyo ya Songea ilizinduka na kujaribu kutengeneza nafasi mbili baada ya kulifikia lango la Simba, lakini walishindwa kufunga.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya mabadiliko, ambapo ilimtoa Murshid na kumuingiza James Kotei, na kuongeza kasi kwa timu hiyo.
Emmanuel Okwi aliiongezea Simba ushindi baada ya kufunga bao la tatu katika dakika ya 52 baada ya mabeki wa Majimaji kushindwa kuokoa mpira wa kona uliochongwa na Kichuya.

Okwi alifunga bao la nne likiwa la pili kwake katika dakika ya 68 akipokea pasi safi ya Bocco, ambaye alifanya kazi ya ziada kuwatoka mabeki wa Majimaji kabla ya kutoa pasi kwa mfungaji.

Okwi ameendelea naye kuzidi kujichimbia kileleni katika mbio za kusaka kiatu cha dhahabu baada ya kufikisha mabao 12 hadi sasa.
Vikosi vilikuwa;Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Asante Kwasi, Juuko Murshid/James Kotei, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Emannuel Okwi, Said Ndemla, John Bocco, Shiza Kichuya/Laudit Mavugo na Jamal Mnyate.

Majimaji: Salehe Malande, Lucas Kikoti, Mpoki Mwakinyuke, Kenned Kipepe, Paulo Maona, Hassan Hamisi, Peter Mapunda, Yakubu Kibiga, Geofrey Mlawa/Six Mwasekaga, Maccel Bonaventure na Jafar Mohamed.
Katika mchezo mwingine, Singida United jana walishinda kwa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Namfua, Singida.