Wednesday, January 24, 2018

LIGI YA WANAWAKE YA SERENGETI PREMIER LITE KUANZA KUTIMUA VUMBI FEBRUARI 24


Ligi ya Wanawake ya Serengeti Premier Lite hatua ya nane bora inatarajia kuanza kutimua vumbi Februari 24, 2018 kwenye viwanja vine.
Mchezo kati ya Kigoma FC na Simba Queens utakaochezwa kwenye uwanja wa Lake Tanganyika ndio utakuwa mchezo rasmi wa ufunguzi.
Mechi nyingine zitakazochezwa katika siku hiyo ya ufunguzi ni Panama watakaokuwa nyumbani Uwanja wa Samora kucheza na Evergreen,JKT Queens wakicheza dhidi ya Alliance kwenye uwanja wa Mbweni.

Mechi nyingine ni ile nitakayowakutanisha Baobab na Mlandizi Queens utakaochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Kabla ya kufika kwenye hatua hiyo,ligi hiyo inayodhaminiwa na bia ya Serengeti Premier Lite kinywaji murua na chenye ubora wa juu ilianzia kwenye hatua ya makundi ikichezwa kwenye Kituo cha Dar Es Salaam kilichotumia Uwanja wa Karume na Kituo cha Arusha kilichotumia Uwanja wa General Tyre.


CAF YAMTEUA MGOYI KUSIMAMIA MECHI YA KOMBE LA SHIRIKISHO BARANI AFRICA KWA VILABU
Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Africa CAF limemteua Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF Ahmed Mgoyi kuwa Kamishna wa mchezo wa Kombe la Shirikisho kwa klabu kati ya AFC Leopards ya Kenya na Fosa Juniors ya Madagascar.

Mchezo huo namba 13 utachezwa nchini Kenya kati ya Februari 9,10 na 11 mwaka huu.
Kwenye mchezo huo waamuzi wote wanatoka nchini Somalia ambapo mwamuzi wa kati ni Abdulkadir Artan Omar,mwamuzi msaidizi namba moja Ali Mohamed Mahad,mwamuzi msaidizi namba mbili Ahmed Abdullah Farah wakati mwamuzi wa akiba ni Hassan Mohamed Hagi.

Mgoyi ni miongoni mwa Wajumbe wa Kamati ya utendaji wa TFF walioteuliwa hivi karibuni kuwa makamishna wa mechi zinazoandaliwa na CAF kwa mwaka 2018 mpaka mwaka 2020 wengine ni Makamu wa Rais wa TFF Michael Wambura,Amina Karuma na Sarah Tchao.

Aidha Rais wa TFF Ndugu Wallace Karia naye mbali ya kuteuliwa kwenye kamati ya mashindano ya fainali za Africa kwa wachezaji wanaocheza ndani CHAN tayari amechaguliwa mara mbili kusimamia mechi za CHAN zinazoendelea nchini Morocco.

Alisimamia mechi ya ufunguzi iliyowakutanisha Wenyeji Morocco na Mauritania Januari 13, 2018 na mchezo wa pili uliochezwa jana Januari 22, 2018 kati ya Namibia na Zambia.


CAF YAJA TANZANIA UKAGUZI MFUMO WA LESENI KWA VILABU
Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Africa CAF litafanya ukaguzi wa mfumo wa leseni kwa vilabu(Club Licencing) kwenye upande wa miundo mbinu.
CAF watafanya ukaguzi huo wa kutembelea na kutazama miundo mbinu ili kuhakikisha mfumo huo unatekelezeka ipasavyo kwa kuanzia na mtazamo wa vigezo vya miundo mbinu.

Wakati wa miaka kadhaa ya kuzindua mfumo huo wa leseni kwa vilabu ni wazi changamoto kubwa kwenye Bara la Africa imekuwa ni vigezo vya miundo mbinu ambayo kwenye baadhi ya viwanja vinavyotumika wakati wa mashindano imekuwa ikitoa taswira isiyo nzuri kwa mashindano ya CAF.
Kwa mwaka huu 2018 wameandaa ukaguzi kutembelea klabu zote zitakazoshiriki hatua ya makundi kwenye mashindano ya vilabu ya CAF wakijielekeza kwenye kiwango na ubora wa viwanja vya kucheza mechi na viwanja walivyochagua kwa mazoezi.

Caf watachagua kundi la wakaguzi watakaotembelea kwenye klabu za kila mwanachama wake ili kukusanya ripoti itakayowasilishwa na moja kati ya ripoti hiyo ni miundo mbinu ya Uwanja,ripoti itakayothibitisha kama uwanja umefikia kwenye mahitaji ya juu ya kutumika kwa mechi za CAF.

Viwanja ambavyo havitakidhi mahitaji hayo ya juu hautaidhinishwa kutumika kwa mashindano na hautatumika kwa mchezo wowote wa hatua hiyo ya makundi kwa mashindano ya klabu kwa mwaka huu 2018.


UKAGUZI WA VIWANJA KOMBE LA SHIRIKISHO LA AZAM VITATU KUTOTUMIKA HATUA YA RAUNDI YA TATU
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF limefanya ukaguzi wa viwanja vinavyotumika kwa kombe la Shirikisho na kuzuia viwanja vitatu kutumika kwa mechi zinazofuata za hatua ya raundi ya tatu.

Viwanja ambavyo havitaweza kutumika kwa raundi hiyo ya tatu ni pamoja na Uwanja wa Nachingwea unaotumiwa na Majimaji Rangers ambao watalazimika kwenda Ilulu Lindi kucheza mchezo wake na Mtibwa Sugar kwenye raundi hiyo.

Uwanja mwingine ni uwanja wa CCM Mkamba Morogoro unaotumiwa na timu ya Shupavu nao hautatumika kwa raundi hiyo na badala yake Shupavu watautumia Uwanja wa Jamhuri Morogoro kwa mchezo wake na Azam FC.

Nayo timu ya Ihefu ya Mbarali haitatumia Uwanja wake kwa raundi ya tatu dhidi ya Yanga na badala yake mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Mbeya.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA TFF