Saturday, February 3, 2018

COASTAL UNION NA KMC ZAPANDA LIGI KUU


TIMU za Coastal Union ya Tanga na KMC ya Kinondoni jijini Dar es Salaam jana zilikata tiketi ya kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao kutoka katika Kundi B baada ya kushinda mechi zao za mwisho.
Coastal Union imerejea katika ligi hiyo baada ya kuifunga Mawenzi 2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa, huku KMC ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Mlale kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Kwa matokeo hayo, KMC inaongoza kundi hilo kwa kuwa na pointi 28 ikifuatiwa na Coastal Union yenye alama 26, huku JKT Mlale wakibaki na pointi zao 25 na Polisi Dar es Salaam wameshuka daraja baada ya kumaliza wakiwa na pointi tano tu.
Katika mchezo huo, Coastal Union waliandika bao la kwanza katika dakika ya 24 lililofungwa kwa penalti na Raizin Hafidh baada ya kuchezewa rafu.
Hatahivyo, mashabiki wa Mawenzi waliwarushia mawe wachezaji wa Coastal Union wakati wakishangilia bao hilo na kuzua mtafaruku.
Ulinzi uliimarishwa baada ya vurugu hizo kufuatia kuongezwa kwa askari wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia, FFU.Ukongwe wa Athuman Idd Chuji pamoja na kipa Hussein Sharifu au Cassilas waliibeba timu yao kutokana na uzoefu wao.
Dakika ya 72 ya mchezo huo, Chuji aliipatia Coastal Union bao la pili lililoihakikishia ushindi timu hiyo na kuondoka na pointi tatu muhimu.
Chuji alifunga bao hilo baada ya kucheza kwa utulivu zaidi baada ya kupata mpira uliopigwa na Andrew Simchimbi na kuokolewa na mabeki wa Mawenzi na kumkuta mfungaji aliyeujaza wavuni.
Mashabiki wa timu hiyo walikuwa wakimshangilia Chuji kwa kumuita `Babu, Babu, Babu’.
Katika matokeo mengine ya kundi hilo, Polisi Tanzania ilibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mufundi huku Mbeya Kwanza wakiibuka na ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Polisi Dar es Salaam.
Timu hizo mbili zinaungana na JKT Tanzania iliyokuwa ya kwanza kupanda daraja kutoka katika Kundi A huku mechi za kundi hilo zikitarajia kumalizika Jumatatu huku zile za Kundi C zitaisha kesho Jumapili.