Sunday, February 11, 2018

FULL TIME: YANGA 1-0 ST LOUIS


YANGA leo imeifunga Saint Louis ya Shelisheli bao 1-0 lakini imejiweka pabaya kwani sasa italazimika kushinda ama kulinda bao lake ili wenyeji wasipate bao katika mechi ya marudiano Shelisheli wiki ijayo.
Juma Mahadhi ndiye aliyeifungia Yanga bao hilo pekee katika mechi hiyo ya awali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mahadhi alifunga bao hilo katika dakika ya 67 ikiwa ni dakika moja tangu alipoingia uwanjani kuchukua nafasi ya Ibrahim Ajibu.
Mahadhi alifunga bao hilo akiunganisha kona iliyochongwa na Geofrey Mwashiuya.
Mapema dakika ya 24 Obrey Chirwa aliikosesha Yanga bao baada ya mkwaju wa penalti aliopiga kwenda pembeni.Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi baada ya Hassan Kessy kuangushwa eneo la hata
Kwa ujumla katika mechi ya jana, wapinzani wa Yanga waliingia kuzuia hali iliyowapa ugumu washambuliaji wa Yanga kuipenya ngome yao, hasa katika kipindi cha kwanza.
Katika kipindi hicho cha kwanza, Yanga ilikosa mabao katika dakika ya 16, Pius Buswita alikosa baada ya kupiga vibaya mpira wa kona, Emmanuel Martin naye akiwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga katika dakika ya 19, alipaisha mpira.

Ajibu naye alishindwa kufunga dakika ya 41 na dakika ya 43, Papy Tshishimbi naye alishindwa kufunga akiwa kwenye nafasi nzuri ya kufanya hivyo.
Kutoka kwenye uwanja wa Amaan Zanzibar, mwandishi Wetu Mwajuma Juma anaripoti kuwa wenyeji JKU wametoka suluhu na Zesco ya Zambia katika michuano hiyo.